Ajenda ya mageuzi ya vijana tangu uhuru imekuwa ya kuungwa mkono, kufundisha maadili, ulengaji mahiri wa kiufundi, utendaji wa mikakati, mawasiliano na ubia madhubuti.
Maendeleo na juhudi za kuimarika zimekuwepo, zipo na bado zitakuwepo. Kiufupi nchi imepiga hatua Kwa asilimia kubwa kwa ajenda ya mageuzi ya vijana tangu tangu kupata uhuru.
Kwa mazingira ya kawaida kuna maendeleo mengi mno juu ya mageuzi ya vijana. Kwanza nchi imejikita katika mwendelezo mzuri wa elimu kwa vijana kutoka kwa wale wenye umri mdogo mpaka kwa wale ambao wamebalehe na kukomaa. Pili ni kuwa vijana wanapoikumbatia elimu ya upili (sekondari) walimu huanza kuwapa wasia kuhusiana na maisha pamoja na masomo yao. Hapa ndipo vijana wengi hupewa maelezo juu ya mstakabali wa kuchangua ‘kozi’ ambazo watafanya vyuoni. Hawaambiwi tu uzuri wa masomo fulani vyuoni ila pia huelezewa manufaa ya masomo hayo maishani mwao.
Kutokana na serikari kuwekeza katika mazingira ya elimu kwa kukarabati au kujenga miundo mbinu, maendeleo kwenye ajenda ya mageuzi ya vijana yameimarika.
Ufadhili wa vijana katika masomo yao kwenye vyuo vya anuai na vyuo vikuu ni jambo ambalo serikali imewekeza kwa asilimia kubwa ili kutimiza ajenda ya mageuzi ya vijana. Kwa serikali kuu imekuwa wajibu kwani isipozifadhili shughuli za vijana masomoni makadirio yao ya siku za usoni yatafeli. Hii ni kupitia ufadhili wa HELB, ‘Capitation’ pamoja na basari zinazopeanwa na viongozi wa maeneo bunge, wadi pamoja na magavana katika sehemu husika.Serikali imekuwa ikishirikiana na mashirika ya kibinafsi ili kutoa ufadhili wa elimu ya ziada ndani na nje ya nchi kwa vijana walio na uwezo wa kubuni vitu tofauti tofauti. Wapo baadhi ya vijana ambao huchuma tonge kubwa kwa uvumbuzi na ubunifu wao kwa juhudi za kufadhili kimasomo zaidi na serikali.
Serikali ya Kenya imeweka sera za kuhakikisha ajenda ya mageuzi ya vijana inafanikishwa.Hii ni kupitia kuwapa nafasi za uongozi serikalini ili kuwapevua macho na kuwathamini kwa shughuli tofauti kwa lengo la kukuza viongozi wa baadaye.Kupitia nafasi hizi adhimu serikali inaimarisha ajenda za mageuzi za vijana. Na shughuli za vijana uongozini nchini zimeongezeka mno kushinda awali. Asilimia kubwa ya vijana imejikita katika kugombea nyadhifa mbalimbali za uongozi katika siasa za nchi hii tukufu. Pia serikali imeanzisha mashirika ya kuwafunza vijana adabu pamoja na kazi zingine nyingi ambazo zina manufaa kemkem. Lipo shirika la National youth service(NYS) ambalo limetengwa mahsusi kwa vijana kuweza kufanyishwa mazoezi na baada ya miezi sita hupelekwa vyuoni ama vyuo vya anuai kusomea kozi ambazo wanazipendelea. Hii imeimarisha nidhamu kwa vijana wengine nchini. Wengi wametimiza ndoto zao kupitia shirika hili.
Aidha serikali imependekeza sera zipangwe kwa kuzingatia matakwa ya vijana kuanzia ngazi ya kitaifa hadi mashinani, pia kuna sera za kubuni pragramu zinazolenga vijana katika maeneo wanayoishi ili kutambua haki za vijana na maendeleo yao kwa kuzingatia kwamba wana ndoto zao ambazo wangependa kutimiza.
Serikali inatumia takwimu za sasa na kutumia ujuzi wa vijana na uzoefu wao katika kupanga,kutekeleza na kutathmini sera za vijana.Ujuzi wa vijana hutumiwa kwingi sana nchini.Wapo vijana ambao ni wazuri mno katika shughuli za kupanga na kupamba majukwaa ya matamasha.Matamasha hayo huwapa vijana ajira kwingi nchini.Wapigaji picha kwenye hayo matamasha asilimia kubwa huwa ni vijana.Hii pia hupigiwa mfano,vijana wanapoteuliwa kujiunga na jeshi la nchi.Wengi huwekwa mahali salama kulingana na talanta zao au ubunifu wao.Wapo ambao watapelekwa kwenye taaluma ya kupika jeshini.Wengine huingia jeshini kama madereva n.k.
Mathalani vijana wengi ni walioko vyuoni wengi wao huwa hawana muda wa kujihusisha na mambo yanayowahusu.Kwao huona ni kupoteza muda.Serikali pia imeweka kitengo cha pesa taslimu kwa maendeleo ya vijana ila vijana hawashughuliki kabisa na manufaa ya hizo fedha.
Ijapokuwa serikali inapambana mno kufanikisha ajenda ya mageuzi ya vijana. Kutimiza na kuzingatia matakwa ya sera walizoziweka umekuwa mtihani mgumu sana. Sera za kuwapa vijana asilimia kubwa kwenye ajira ya kazi za serikalini umekuwa mtihani haswa! Kama sio mtihani basi donda ndugu ambalo halisikii dawa kabisa.
Jambo jingine ambalo linazuia maendeleo katika ajenda ya mageuzi ya vijana ni dawa za kulenya. Vijana wengi wamejikita kwenye matumizi ya dawa za kulevya kutokana na shinikizo kutoka kwa vijana wenzao ,uraibu na kukosa cha kufanya. Hizi dawa za kulevya huwapotezea muda wao muhimu ambao wanaweza kuutumia kufanikisha ajenda ya mageuzi kwa vijana nchini.
Aidha vijana wengi wanapenda kutumia muda wao mwingi kwenye mitandao ya kijamii pasi na upangaji mzuri wa mikakati yao juu ya mambo ya msingi maishani mwao. Ili kukuza na kupata maendeleo endelevu katika ajenda ya mageuzi ya vijana nchini siku za usoni. Serikali inafaa kuwekeza mno katika masuala yenye faida kwenye mitandao ya kijamii kwa kuwa vijana wengi wametekwa na mitandao.
Serikali pia inafaa kuweka njia mwafaka za kuweza kutimiza sera ambazo inaweka katika ajenda za mageuzi ya vijana. Sera nyingi zinazowekwa hazifatiliwi. Kando na hayo serikali inafaa kufungua vituo vingi zaidi vyenye manufaa kwa nchi na kwa vijana kwa mafunzo mahsusi katika idara zote za kazi nchini. Kwa kufanya hivyo vijana wengi watajitambua na watakuwa na uwezo wa kuchapa kazi tofauti tofauti bila kulia eti hakuna kazi kwa vijana nchini.
Mhandishi: Agadias Ikoha Yambasa, Mwanafunzi, Sigalagala National Polytechnic